Mwili wa Kapteini John Damian Komba ukiagwa.
NIKIMYA Milele. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya msiba mkubwa uliotingisha nchi, kufuatia kufariki ghafla, kuagwa na hatimaye kufanyika kwa mazishi ya Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteini Mstaafu wa Jeshi, John Damian Komba katika Kijiji cha Lituhi, kilichopo katika mwambao wa Ziwa Nyasa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Kapteni Komba aliyekuwa pia ni mtunzi mahiri wa nyimbo na mwimbaji hodari wa kwaya, kabla ya mazishi yake, aliagwa katika tukio la kitaifa lililofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wote wakubwa, wakiongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wake, Dokta Ghalib Bilal na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda.
Rais Kikwete akiwa na huzuni.
Wengine waliokuwepo katika tukio hilo lililorushwa moja kwa moja na kituo cha taifa cha televisheni cha TBC 1, ni wanaotajwa kuwania nafasi ya kuteuliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu ujao kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ambaye ni mbunge wa Sengerema.
Rais mstaafu Benjamin Mkapa akiuzunika.
Pia alikuwepo Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dokta Wilbroad Slaa, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia wanaowakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wabunge kutoka vyama vyote vya siasa, majaji wa Mahakama Kuu, marais wawili wastaafu, Ally Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa na viongozi waandamizi wa zamani na sasa katika serikali.
Ingawa tukio hilo lilikuwa ni la huzuni, lakini bado wagombea hao wa Urais waliwateka mamia ya waombolezaji kutokana na wapambe wa pande zote mbili kujawa na hamasa walipokuwa wakipita au majina yao kutajwa na MC wa shughuli hiyo.
Kwa nyakati tofauti, wawania uongozi hao walionekana nyumbani kwa marehemu, Mbezi Beach na baadaye katika ukumbi wa Karimjee.
Waombolezaji wakiuaga mwili wa marehemu kwa simanzi kubwa.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa wanasiasa wa kambi zote kuelezea kuguswa kwao na msiba huo wa mmoja wa watunzi hodari zaidi nchini, upande wa wasanii, walionekana kukwepa kuhudhuria hafla hiyo, tofauti na inavyotokea pale mwenzao anapofariki dunia. Ukiondoa wasanii walioalikwa kuimba, wakiwemo wa dansi, Bongo Fleva na Bongo Movies, hakukuwa na idadi kubwa ya mastaa hao kama ilivyotegemewa.
Ilielezwa chinichini kuwa wasanii hao ambao mara zote hushindana kwa vituko, vibweka na matukio, walihofia kufunikwa na wanasiasa, ambao bila kujali tofauti zao za kiitikadi, waliomboleza kwa uzito uliostahili.
“Hawa sijui Bongo Movies, sijui Bongo Fleva hapa leo hakuna cha staa wala nini, mastaa wenyewe wanasiasa wamejazana, unafikiri wangekuja hapa wangemdengulia nani, wao ndiyo wangelazimika kuwa wanyonge na hivyo wanavyopenda kujikweza, wameogopa,” alisema mmoja wa waombolezaji hao.
Komba alitarajiwa kuzikwa jana katika Kijiji cha Lituhi, kilichopo katika mwambao wa Ziwa Nyasa wilaya ya Mbinga.Mungu ailaze roho ya marehemu Komba mahala pema peponi, Amina-Mhariri.
Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Mbinga Mhashamu John Ndimbo akiongoza ibada ya mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damiano Komba wakati wa ibada ya mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma leo.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damiano Komba wakati wa ibada ya mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa ,Mkoani Ruvuma.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi marehemu Kapteni John Damiano Komba wakati wa ibada ya mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake Lituhi wilayani Nyasa, Mkoani Ruvuma.
Post a Comment